Blogroll

Wednesday, June 12, 2013

CCM ‘yammwaga’ Warioba

Picha ya mojawapo ya mandhari za kitalii nchini Tanzania ambazo zinavutia kwa mwonekano wake.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeyakataa baadhi ya mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya yaliyotangazwa na Jaji Joseph Warioba hivi karibuni, ambayo pamoja na mambo mengine, ilipendekeza muundo wa serikali tatu.

Taarifa kutoka ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho (CC), iliyoketi juzi usiku chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, zimeeleza kuwa wajumbe wake walikubaliana kwa kauli moja kuzingatia mapendekezo ya kamati ndogo iliyoundwa na Halmashauri Kuu ambayo Mwenyekiti ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, yaliyopendekeza taifa la Tanzania kuundwa kwa serikali mbili.

Kamati ya Chenge iliundwa Novemba mwaka jana, kwa madhumini ya kuandaa mapendekezo ya chama hicho ya muundo wa Katiba mpya ya Tanzania.

Taarifa zimeeleza kuwa wajumbe wa CC walijadili kwa kina muundo wa serikali tatu na kuuona hauna manufaa kwa taifa kama ilivyopendekezwa na kamati ya Chenge na hivyo walifikia uamuzi wa kuikataa.

Hata hivyo, ilikubaliwa na wajumbe wote kuwapa nafasi wanachama wa chama hicho ngazi ya matawi na wilaya kuijadili rasimu hiyo, kabla chama hakijachukua uamuzi wa mwisho.

Tume ya Jaji Warioba katika mapendekezo yake ya muundo wa utawala, ilipendekeza kuwepo serikali tatu; ya Zanzibar, Tanzania Bara na Serikali ya Shirikisho, jambo ambalo limeibua mjadala, huku makundi mbalimbali ya watu wakipinga pendekezo hilo.

Uchunguzi wa MTANZANIA Jumatano, umeonyesha kuwa wakati CCM kikichukua uamuzi huo, wananchi wengi Wazanzibari wamegawanyika katika makundi mawili kuhusu muundo wa utawala. Wanachama wa CCM Zanzibar na wale wanaounga mkono itikadi za chama hicho wanataka muundo wa serikali mbili, huku wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na wale wanaounga mkono itikadi za chama hicho wakitaka muundo wa muungano uwe wa Mkataba.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wafuasi wa CCM na CUF, kwa upande wa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Bara na Visiwani, wao wanataka muundo wa serikali tatu ambazo ni ya Tanganyika, Zanzibar na Shirikisho.

Mkanganyiko unaoonekana katika serikali tatu, ni namna ya uendeshwaji wa serikali ya Shirikisho, ambapo wachumi, wanasiasa na wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa haitaweza kujiendesha kwa sababu haitakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato.

Wanazuoni mbalimbali waliozungumza na gazeti hili na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba mpya, wameeleza kuwa licha ya Jaji Warioba kueleza kuwa serikali ya shirikisho itakuwa na uwezo kukopa, haitakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato, jambo ambalo litaiondolea uwezo wa kujiendesha na kusimamia mambo saba ya muungano ambayo yameainishwa kwenye rasimu ya Katiba.

Wachumi na wachambuzi wa masuala ya siasa, wameeleza kuwa kwa mujibu wa Jaji Warioba, chanzo cha uhakika cha mapato ya serikali ya shirikisho kitakuwa kodi ya bidhaa ambayo kulingana na mwenendo wa uchumi wa taifa, haitaweza kubeba gharama za uendeshaji wa serikali ya muungano.

“Kodi ya bidhaa ambayo ndiyo itakuwa chanzo cha mapato cha serikali ya shirikisho, haitaweza kubabe gharama za uendeshaji wa serikali ya shirikisho, kwa sababu hiyo itakuwa haina uchumi, haitaweza kujiendesha.

“Serikali ya shirikisho itakuwa inasimamia sarafu ya Zanzibar na Tanganyika, ambayo uimara wake utategemea uchumi wa nchi hizo. Kila nchi itakuwa na sera zake za kiuchumi na sera za kisayansi katika kujisimamia. Nchi hizi zitakuwa na chumi mbili tofauti, wingi wa watu, rasilimali tofauti na ukubwa wa ardhi ambao haulingani, kwa maana hiyo hata uchumi utakuwa tofauti.

“Sasa shirikisho hilo litakuwa halina tofauti na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, inayotegemea mapato ya ushuru,” alisema mchumi mmoja aliyezungumza na gazeti hili.

0 comments:

Post a Comment